Read this blog in English.

Kuluthum Mbwana anakumbuka siku ambapo wawekezaji wa bayofueli walifika kijijini mwake cha Vilabwa, takribani kilomita 70 magharibi mwa jiji kuu la Tanzania. Alisema wawekezaji hao waliahidi kuleta ajira zinazohitajika sana, shule na vituo vya afya katika jamii yake, kwa kubadilishana na zaidi ya hekta 8,000 (ekari 19,800 ) za ardhi katika vijiji 11, ikiwemo kijiji cha Vilabwa, katika Wilaya ya Kisarawe

Mbwana aliamini kabisa kuwa maisha yake yatakuwa bora. Hatimaye watoto kotekote kijijini mwake wangepata fursa ya kusomea katika shule halisi. Majirani wenye magonjwa wangepata matibabu kutoka kwa wauguzi au wafanyakazi wa afya ya jamii waliohitimu mafunzo. Ajira mpya zingeleta fedha zaidi kwenye kijiji hicho na kuimarisha uchumi.

Lakini Mbwana akasema kwamba baada ya kampuni ya Sun Biofuels ya Uingereza kukamilisha mkataba wa ardhi kati yake na Serikali ya Tanzania mwaka 2009, kampuni hiyo ilitelekeza ahadi zake walizomwahidi yeye pamoja na wanakijiji wengine wa Vilabwa. Familia zilizouzia kampuni hiyo mashamba yao hazikupata malipo ya haki kwa ardhi yao. Mishahara kutokana na ajira za Sun Biofuels ilikuwa ya chini sana isiweze kufidia mapato ambayo wanakijiji walipoteza baada ya kuiuzia kampuni hiyo mashamba yao. Isipokuwa tu kisima kimoja kifupi, barabara ya maramu na mbao chache za darasani za kuchukulika, Sun Biofuels haikuleta huduma za kijamii kwenye kijiji cha Mbwana na kwa jamii jirani katika Wilaya ya Kisarawe.

Kuluthum Mbwana. Photo by TGNP Mtandao
Kuluthu Mbwana

Kwa kusikitisha, yaliyompata Mbwana ni mambo ya kawaida barani Afrika. Ardhi inapozidi kupoteza rutuba, mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la idadi ya watu vinapozidi kuilemea ardhi ambayo huwalisha mamilioni ya watu, kampuni za kimataifa pia zinang'ang'ania kudhibiti maeneo makubwa ya ardhi. Wanapobanwa na mikazo hiyo, jamii nyingi maskini zinazoishi vijijini huondolewa kwenye makazi yao au huamua kuuza ardhi inayomilikiwa na jamii kwa pamoja. Na mara nyingi wanawake ndio huumia zaidi.

Katika nchi jirani ya Msumbiji, Leonor dos Anjos pia anakumbana na ahadi ambazo hazijatimizwa. Mwaka wa 2016, mradi wa mamilioni ya dola wa kujenga daraja linaloning'inia uliihamisha familia yake na kuilazimisha jamii yake ya Malanga kwenda kuishi katika maeneo matatu tofauti-tofauti. Akiongea na shirika lisilopata faida liitwalo Centro Terra Viva la Msumbiji, dos Anjos alisema kwamba kampuni inayomilikiwa na serikali na ambayo inasimamia ujenzi wa daraja hilo, Maputo Sul Development Company, iliahidi kuwapa ardhi mpya iliyotayarishwa, kujenga barabara inayounganisha makazi yake na barabara kuu na kufidia familia hizo nyumba zao. Lakini kama ilivyo na Sun Biofuels, dos Anjos anaamini kuwa kampuni ya Maputo Sul haikutimiza ahadi zake na ilikandamiza familia maskini kwa kuwatwika mizigo ya kifedha ambayo haikutarajiwa.

Uchunguzi mpya kutoka kwa WRI unaonyesha kwamba licha ya ahadi ya kikatiba za kuwa na usawa wa kijinsia, serikali nchini Tanzania na Msumbiji haziwalindi wanawake maskini wa vijijini kutokana na biashara za ardhi zenye kudhuru. Kushindwa kwa maofisa wa serikali kuziba mapengo katika sheria za ardhi na kukarabati sheria ambazo si fanisi kunawapunja wanawake, ambao hupokea malipo madogo sana au hawapokei chochote kwa ajili ya ardhi ya familia zao. Juhudi za serikali za kukuza sauti zao katika maamuzi yanayohusu ardhi ya jamii pia hazifikii malengo.

Wamepunjwa katika Biashara ya Ardhi

Ingawa sheria za ardhi za Tanzania na Msumbiji zinawahitaji wawekezaji wazifidie jamii na nyumba zilizoathiriwa wanaponunua ardhi inayomilikiwa na jamii kwa pamoja, sheria duni au ambazo hazitekelezwi ipasavyo huwapunja wanawake, ambao mara nyingi hupokea malipo madogo sana, au hawapokei chochote, kwa ajili ya ardhi yao.

Malanga women in Mozambique.

Kihususa, lugha isiyoonyesha usawa wa kijinsia huwabagua wanawake bila kukusudia kwa kuzitaka kampuni kulipa fidia kwenye ngazi ya kaya. Kwa kuwa kulingana na desturi wanaume ndio vichwa vya kaya katika nchi hizo mbili, ni wao pekee wanaweza kuwasilisha madai na kuchukua malipo kwa niaba ya familia zao. Kwa mfano, chini ya asilimia 15 ya wale waliopokea fidia kutoka kwa Sun Biofuels katika kijiji cha Vilabwa ni wanawake. Katika kijiji cha Malanga, wanaume kadhaa waliotengana na wake zao na kuondoka kwenye jamii walipokea hundi ambazo zilipasa kwenda kwa wake zao kwa sababu serikali bado iliwaona kuwa vichwa vya kaya zao.

Lakini hata wakati ambapo wanawake wanafaulu kupata fidia kwa ajili ya ardhi yao, wengi hupokea malipo ya chini ikilinganishwa na wanaume walio kwenye jamii zao. Kwa mfano, katika kijiji cha Vilabwa, wanaume walipokea pesa mara tatu hadi sita zaidi kuliko wanawake kwa ajili ya ardhi yao.

Tofauti hizo hutokea kwa sababu kadhaa: Kampuni huwalipa tu wale wanaomiliki ardhi kisheria, na wanawake wengi, kinyume na wanaume, hawana umiliki rasmi wa ardhi yao. Viwanja wanavyomiliki ni vidogo navyo hutoa mazao madogo ya kilimo ikilinganishwa na viwanja vya wanaume. Na wanawake wengi hulima mazao ya chakula, kama vile mihogo au mahindi, ambayo mara nyingi kampuni huyakadiria thamani ya chini au hayahesabii thamani yoyote.

Wanaathiriwa Vibaya Jamii Zinapohamia Kwenye Makazi Mapya

Wanawake pia hupata magumu kuliko wanaume katika kuanza maisha mapya na kuanzisha njia mpya za kupata riziki wakati kampuni zinapovihamisha vijiji au kuzipa jamii makazi mapya. Jamii zinapohamishwa, mara nyingi wanawake hupoteza uwezo wa kutumia rasilimali za kijamii — kama vile misitu, mito na malisho — na bado wanawajibika kuteka maji, kuni, chakula cha mifugo na mitishamba kwa ajili ya familia zao. Uwezo hafifu wa kufikia rasilimali hizi kunaweza kuongezea wanawake mizigo, kuhatarisha usalama wa chakula na kuzidisha uwezekano wa kudhulumiwa.

Wanapokabili hali hizi mpya gumu, wanawake wengi huona kwamba mitandao ya kijamii wanayotegemea hudhoofika wanapohama. Kwa mfano, mara nyingi wasichana hukusanya kuni na kuteka maji wakiwa kwenye vikundi, ilhali akina mama huwategemea majirani au jamaa zao kuwatunzia watoto. Wakati wanawake wanapotenganishwa na mitandao yao, hawana tena mifumo ya utegemezi wanayohitaji ili kukabiliana na changamoto za kila siku na kutekeleza majukumu yao mengi ya kaya.

Wanatengwa Kwenye Maamuzi ya Jamii kuhusu Ardhi

Women in rural Tanzania. Flickr/CIAT

Kujumuisha sauti za wanawake katika mashirika ya kijamii yanayofanya maamuzi kunaweza kusaidia jamii kutatua ukosefu wa usawa wa kijinsia katika fidia za ardhi na miradi ya makazi mapya kwa kuwapa fursa ya kusema “ndio” au “la” kwa mapendekezo yanayotolewa kuhusu kuuza ardhi, kusaidia kujadili michakato ya tathmini za kampuni ili kuhakikisha kuwa wawekezaji hawaondoi mali zao kwenye tathmini za thamani, na kuibua masuala maalum kuhusu mipango ya kuhamishiwa mahali kwingine. Lakini katika nchi hizi mbili, juhudi za serikali za kuimarisha uwakilishi wa wanawake hazifikii malengo.

Nchini Tanzania, sheria zinaamrisha wanawake wakuwepo katika mabaraza ya vijiji, lakini fungu la wanawake ni viti vichache tu, hali ambayo hufanya iwe rahisi mkutano kufikia akidi bila kuwashirikisha wanawake.

Vivyo hivyo, nchini Msumbiji, lugha isiyo hususa katika sheria za ardhi, kama vile “wawekezaji wanapaswa kushauriana na jamii,” haiwatwiki wawekezaji wajibu wa kuwajumuisha wanawake katika mchakato wa mashauriano. Maamuzi mengi makubwa kuhusu ardhi, ikiwemo kuuza ardhi ya jamii kwa wawekezaji, hufanywa na viongozi wanaume au katika mikutano inayoshirikisha wanaume pekee. Hata kama wanawake wanahudhuria, wengi hukaa kimya kwa sababu ya dhana isiyo wazi kwamba wanaume huzungumza kwa niaba ya jamii nzima.

Suluhisho

Flickr/USAID

Maisha na riziki ya wanawake wengi vijijini, kama ya Mbwana na dos Anjos, hutegemea ardhi yao karibu kwa kila kitu. Kuendeleza haki zao za ardhi — kuanzia usawa kuweko katika uuzaji wa ardhi hadi uwakilishi bora katika ufanyaji maamuzi katika jamii — ni muhimu katika kuafikia usawa wa kijinsia, sio tu nchini Tanzania na Msumbiji, bali katika nchi zote barani Afrika.